Tuesday, July 24, 2012

ZITTO AREJESHA PENZI LA WEMA NA DIAMOND!!!!!MBUNGE wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, ametajwa kuwa kichocheo cha kurejea kwa penzi la vijana wenye umaarufu mkubwa nchini kwa sasa, Nasibu Abdu Juma ‘Diamond’ na Wema Isaac Sepetu.
Uwazi, lina mkanda wa video, unaowaonesha Diamond na Wema pamoja kwa mara ya kwanza, baada ya muda mrefu wa kutupiana maneno mengi ya kashfa, huku kila upande ukimshusha hadhi mwenzake.
Diamond na Wema, walinaswa kwenye Tamasha la Kigoma All Stars, lililoandaliwa na Zitto kisha kufanyika Julai 17, mwaka huu kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.
Shukurani kwa Zitto, kwani kupitia tamasha hilo, Diamond na Wema, waliweza kudhihirisha kwa kila mtu kwamba uhusiano wao sasa umerejea upya kwa kuambatana kimahaba ndani ya Mkoa wa Kigoma.
SAFARI ILIVYOKUWA TAMU
Watu wengi wakijua kwamba kuna uhasama mkubwa kati ya Wema na Diamond, Julai 17, mwaka huu, ilikuwa ni mshangao wa aina yake kwa waliokuwepo Uwanja wa Ndege wa Mkoa wa Kigoma, baada ya vijana hao kushuka wakiwa wameongozana.
Diamond akiwa amevaa shati jekundu na tai nyeusi, chini akiondokea suruali ya jeans rangi ya bluu iliyopaushwa kimodo, huku Wema akitokelezea kwa koti la rangi ya maziwa, ndani blauzi nyeusi, halafu wote wameyaficha macho yao kwa miwani nyeusi, waliwaka vilivyo ndani ya Ujiji, Kigoma.
Baada ya kuwasili Kigoma, Wema na Diamond walielekea Hoteli ya Tanganyika Beach (ipo ufukweni mwa Ziwa Tanganyika) ambako walipata pumziko walilohitaji kabla ya nyota huyo wa wimbo wa Mbagala, hajaelekea Uwanja wa Lake Tanganyika kwenye Tamasha la Kigoma All Stars a.k.a Leka Dutigite.
WEMA ALIFUATA NINI KIGOMA?
Minong’ono ilitawala kila kona ya Mkoa wa Kigoma kwamba Wema amekwenda kuwakilisha Leka Dutigite, hivyo wakataraji kumuona Uwanja wa Lake Tanganyika, akitoa sapoti yake kwenye tamasha hilo.
Wapo ambao waliacha shughuli zao kwa ajili ya kwenda kumuona Wema tu uwanjani lakini waliambulia patupu, kwani mrembo huyo hakuonekana kabisa.
Kutokana na hali hiyo, wale waliovumisha stori kwamba Wema amekwenda Kigoma a.k.a Lwama, walionekana wazushi wasiofaa kusikilizwa, bila kujua kwamba mtoto alijificha ndani ya Hoteli ya Lake Tanganyika Beach.
HAKIKA WANAPENDANA
Kama ukaribu wao ulisababishwa na tamasha lililoandaliwa na Zitto peke yake, basi wangekuwa na muonekano ‘feki’ sehemu chache wanazopita lakini kinyume chake wao walithibitisha wanapendana haswaa!
Diamond, alishindwa kujichanganya na wasanii wenzake aliokuwa nao kwenye shoo ya Kigoma kama akina Said Juma ‘Chegge’, Peter Msechu, Banana Zorro, Mwasiti Almasi na wengineo, badala yake muda mwingi aliutumia kuwa umbali wa mita sifuri kutoka alipo Wema.
Mtundu’ wa nyimbo mbili mpaka sasa, Nai Nai na Baadaye, Omar Faraji Nyembo ‘Ommy Dimpoz’, ndiye pekee aliyekuwa jirani na vijana hao maarufu, walioamua kurejesha penzi lao kupitia mwavuli wa shoo hiyo.
Kwa upande mwingine, ni kama vile waliamua kwenda kufanya tambiko nyumbani asili kwa mume mtarajiwa, yaani Diamond kwa sababu chimbuko la Wema ni Mkoa wa Tabora, japo baba yake, Balozi Isaac Abraham Sepetu, amejichimbia Zanzibar kwa miaka mingi.
Mtu mmoja, mwenye hulka ya kutopitwa na mambo, akamueleza ripota wetu kuwa Julai 18, wasanii hao walikwenda Hifadhi za Gombe na Mahale, mkoani humo lakini jioni yake, Diamond aliongozana na Wema mpaka kwa babu yake, eneo la Ujiji Posta, mkoani humo ambako walisomewa dua na Babu Nasibu.

No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...